Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetangaza mpango maalumu wa kutoa msaada wa kisheria bila malipo kwa watuhumiwa waliokamatwa au kufunguliwa mashtaka kuhusiana na matukio ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025, likishirikiana na mashirika ya haki za binadamu ikiwamo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 9, 2025 na Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi, msaada huo unalenga kuhakikisha watuhumiwa wanapata uwakilishi wa kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017.
“Lakini pia msaada huo wa kisheria unatolewa kwasababu watuhumiwa wengi wanatoka familia zenye kipato cha chini zisizokuwa na uwezo wa kulipa gharama za mawakili. Haki ya kila mtu kupata uwakilishi wa kisheria ni ya msingi na ni haki ya kikatiba”, imeeleza taarifa hiyo.
TLS imeorodhesha zaidi ya mawakili 40 walioteuliwa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salaam, Iringa, Tabora, Njombe, Morogoro, Kigoma, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Songwe, Mbeya, Mbeya na Mara.
Katika Dar es Salaam pekee, zaidi ya kesi nne zimeorodheshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu zikiwa na idadi tofauti ya watuhumiwa wakiwemo 95, 76, 34 na 13 ambapo mawakili maarufu kama Peter Kibatala, Mpale Mpoki, Hekima Mwasipu na Fredrick Msaki wametajwa miongoni mwa wanaotoa msaada huo.
Aidha, TLS imezikumbusha familia za watuhumiwa kuwa hazikatazwi kuwa na mawakili binafsi, lakini msaada huo wa bure unalenga kuhakikisha watuhumiwa wote wanapata utetezi sahihi bila vikwazo vya kifedha.
“TLS tunawashukuru mawakili wote ambao wamekubali na wako tayari kujitolea kutoa msaada wa kisheria nchi nzima. TLS inasisitiza mawakili wanaotoa msaada wa kisheria wasisumbuliwe wala kutishiwa wanapokuwa wanatimiza majukumu haya kama maafisa wa mahakama”, imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Familia zinazohitaji msaada wa kisheria zimetakiwa kuwasiliana na TLS kupitia WhatsApp namba 0777 815 757 au barua pepe president@tls.or.tz
TLS imesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kulinda haki za watuhumiwa na kuimarisha utawala wa sheria katika kipindi ambacho taifa bado linakabiliana na matokeo ya kisiasa na kijamii yaliyofuatia uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.