Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasin, ametoa pole kwa wote walioathirika na matukio yaliyotokea tangu siku ya uchaguzi mkuu wa Tanzania tarehe 29 Oktoba, 2025 akisema matukio hayo yameacha taswira mbaya ikilinganishwa na sifa ya taifa la Tanzania na kuacha historia isiyofutika.
Kupitia taarifa yake kwa umma, Selasin, ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wa upinzani wenye uzoefu mkubwa, ametilia wasiwasi mchakato wa uchaguzi huo akidai kuwa haukuwa huru na wa haki, akitolea mfano hatua ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kususia mchakato huo.
Amesema sababu kubwa ya changamoto hizo ni upinzani dhidi ya mabadiliko muhimu ya kisiasa tangu mwaka 1992. Ameeleza vyombo mbalimbali ikiwamo Tume iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali vilipendekeza mabadiliko ya kikatiba ili siasa zifanyike kwa misingi ya haki na amani, lakini mapendekezo hayo yalipuuzwa. Kwa mujibu wa Selasin, hatua hiyo imesababisha mazingira magumu kwa vyama vya upinzani na kudhoofisha demokrasia nchini.
Selasin pia amekosoa kile alichokiita usumbufu na ukamataji wa wanasiasa wa upinzani, akisema kitendo hicho ni sawa na "kumwaga petroli kwenye moto", hivyo ameitaka serikali kuacha mara moja kuwakamata wanasiasa wa upinzani ili kuimarisha amani na mshikamano wa Watanzania.
Amesema ni wakati sasa kwa viongozi wote wenye uwezo kutumia nafasi zao kuondoa hali hiyo, kwasababu kukaa kimya ni kuchochea mgawanyiko zaidi wa taifa. Aidha amehimiza vyama vya upinzani kushikamana kwa pamoja kutetea haki na kuhakikisha umoja wa kitaifa unadumishwa.
"Mimi nilidhani kwamba katika hali ya namna hii tungeangalia namna ya kuliponya taifa letu, taifa limegawanyika, taifa linavuja damu hadi sasa tunavyoongea miili ya wenzetu haijulikani iko wapi…lakini katikati ya jambo hili bado kuna watu wanakamatwa, bado kuna watu wanasumbuliwa, na bado kuna watu wanasukwasukwa na polisi katika uchungu tulionao", ameeleza.